JAMHURI YA KENYA WIZARA YA KILIMO, UFUGAJI, UVUVI NA UNYUNYIZAJI (MoALFI) IDARA YA SERIKALI YA UVUVI, KILIMO CHA MAJINI NA UCHUMI WA RASILMALI ZA MAJINI (SDFA-BE) RASIMU YA MWISHO YA RIPOTI YA TATHMINI YA KIJAMII MRADI WA MAENDELEO YA KIUCHUMI NA KIJAMII KATIKA SEKTA YA UVUVI WA BAHARINI KENYA (KEMFSED) WARSHA YA KUHALALISHA MOMBASA TAREHE 19-20, JUNI 2019 Utangulizi 1 Serikali ya Kenya inaandaa Mradi wa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii katika sekta ya Uvuvi wa Baharini ( KEMFSED). Mradi wa KEMFSED utadumu kwa muda wa miaka 5. Lengo la jumla la mradi ni kuimarisha manufaa ya kiuchumi na maisha ya wakazi wa pwani kutokana na uvuvi wa baharini na kilimo cha majani huku ukiendelea kulinda rasilimali husika. Idara tekelezi itakuwa Idara ya Taifa ya Uvuvi, Kilimo Maji na Uchumi wa Rasilimali za Maji (SDFA-BE) kwa niaba ya Serikali ya Kenya. Nchini Kenya, gatuzi 5 katika ukanda wa Pwani zimeteuliwa kunufaika na mradi huu, nazo ni Kwale, Mombasa, Kilifi, Tana River na Lamu. Mradi wa KEMFSED unanuia kuziwezesha jamii za pwani kuimarisha usimamizi na uongezaji wa thamani kwenye uvuvi na shughuli za kiuchumi zinazotokana na maliasili ya baharini pamoja na kuboresha upatikanaji wa shughuli mbadala za kiuchumi. 2 Inadhamiriwa kwamba mradi huu utanufaisha serikali ya taifa na zile za gatuzi husika za pwani kwa kuboresha mifumo ya utawala na usimamizi pamoja na mifumo ya uvuvi wa baharini, kuwezesha uwekezaji endelevu katika uvuvi wa baharini na kilimo maji kupitia Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SME) kwa ushirikiano na washirika binafsi watakaohusishwa katika shughuli saidizi kwa wajasiriamali wadogo na wa kati pamoja na kuwezesha uchumi na upatikanaji wa riziki kwa jamii zilizochaguliwa katika kaunti ndogo za pwani. Tathmini ya Kijamii 3 Kwa kuzingatia mwongozo wa Benki ya Dunia, OP4.10, Tathmini ya Kijamii hufanywa kwa ajili ya mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ili kuimarisha muundo wa mradi na kuanzisha ushirikishaji wa jamii zilizotengwa katika mchakato wa utekelezaji na ufuatiliaji wa mradi. Ili kufanya hivi, mchakato wa tathmini ya kijamii huzingatia hali, maoni na mapendeleo ya makundi yaliyotengwa na yaliyo katika hatari ya kuathirika. Lengo la Tathmini ya Kijamii ni kubuni uelewa wa masuala ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni ya Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika kwenye kaunti husika ili kuyazingatia katika mradi wa KEMFSED, lengo ni kuhakikisha kwamba mradi unazingatia mahitaji yao ya ukuaji wa kijamii. Malengo mahususi ya tathmini hii yalikuwa: kuuwezesha mradi kuunga mkono matarajio na mahitaji ya Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika pamoja na watu katika maeneo ya mradi; Kutambua na kuandaa mpango mahususi utakaozuia madhara yoyote yanayoweza kutokana na shughuli za mradi kwa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika na pasipowezekana au pasipotendeka, kupunguza athari au kufidia matokeo ya madhara mbali na kuhakikisha kwamba mradi unawanufaisha Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika kwa usawa na kwa kutumia taasisi zinazoheshimu na zinazoweza kuwahudumia kwa namna iliyogatuliwa. Kwa mradi huu, mpango tofauti hautaandaliwa kwa ajili ya Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika kwa sababu makundi hayo yatalengwa na kunufaika kutokana na vipengele vya mradi huu ili kuhakikisha ustawi wao kijamii na kiuchumi. 4 Tathmini hii ya kijamii ilifanywa katika Makundi tofauti Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika ambayo kwa sasa yanaishi katika wadi za kaunti ndogo zitakazolengwa na utekelezaji wa mradi wa KEMFSED katika kaunti za Kwale, Kilifi, Lamu na Tana River. Utaratibu ulihusu kukusanya data kwa kutumia vyanzo vya asili na vya ziada vya data ili kusaidia katika kuandaa Tathmini ya Kijamii na Muungano wa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika. Data ya ziada ilipatikana kutokana kutoka kwenye machapisho, huku ile ya asili ikikusanywa kwa kushauriana na wadau, mahojiano na wajuzi wakuu, midahalo ya makundi mahususi na uangaliaji nyanjani ulizijumuisha Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika na makundi mengine katika kaunti zilizochaguliwa. Mifumo ya Kitaasisi, Kisera na Kisheria 5 Kuna asasi nyingi nchini zinazolinda haki za Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika. Asasi hizo ni pamoja na Wizara ya Leba na ulinzi wa Jamii; Wizara ya Huduma za Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia inayoratibu mipango ya kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu nchini pia ina jukumu la kukuza usawa wa kijinsia nchini; Tume ya Taifa ya Usawa wa Kijinsia inayohusika katika uhusishaji wa masuala ya jamii za wachache katika maendeleo; Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu nchini Kenya ambayo hufuatilia mashirika ya serikali na kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki; Tume ya Taifa ya Uwiano na Utangamano ambayo kimsingi ina jukumu la kuzuia ubaguzi kwa misingi ya rangi au kabila pamoja na kutetea utangamano miongoni mwa jamii mbalimbali nchini Kenya na vilevile Makavazi ya Kenya ambayo inalinda turathi. Sheria na Mipango ya Kitaasisi kwa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika 6 Katiba ya Kenya ya mwaka 2010 inatambua haki za kijamii, kiuchumi na kitamaduni ya raia wote ilivyoelezwa katika Ibara ya 43. Inatambua watu wa asili kuwa jamii ya wachache ambao wametengwa katika michakato ya kihistoria. Ina fasili pana ya watu waliotengwa inayojumuisha makundi mengi yanayojitambulisha kuwa watu wa asili. Katiba inakataza kubagua makundi yaliyotengwa kwa sababu ya idadi yao ndogo au yale ambayo hayajaweza kuendeleza kikamilifu mifumo au rasilimali zao kushiriki katika maisha ya kijamii na kiuchumi nchini Kenya. Kadhalika, inatambua jamii ambazo zimehifadhi tamaduni na utambulisho wao maalum unaowazuia kushiriki katika maendeleo ya kiuchumi nchini, ikiwa ni pamoja na jamii zinazowinda na kukusanya mazao ya porini, jamii za wafugaji na wavuvi miongoni mwa nyingine. Utambuaji wa Makundi haya Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika unafaa kuchangia katika uhifadhi wa utambulisho wao na kuwawezesha kuhusika kwa usawa katika maendeleo pamoja na jamii nyingine kubwa, ikiwemo kushiriki katika maisha ya kisiasa. 7 Katiba ya Kenya na sheria nyingine husika ina mfanano mwingi na mwongozo wa OP. 4.10. Kuna mfanano kati ya makundi yanayotambuliwa na serikali ya Kenya kuwa yaliyotengwa na yaliyo katika hatari ya kuathirika na yale yaliyosababisha kuwepo kwa mwongozo wa OP 4.10. Vilevile, makundi yanayotambuliwa na serikali na katika muktadha wa miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia yanalingana na makundi ambayo yameainishwa na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu (ACHPR) katika utambuzi wake wa dhana ya uhalisi na kile dhana hiyo inamaanisha katika muktadha wa Afrika. Kijumla, hakuna mgongano kati ya malengo na kanuni kuu za mwongozo wa OP 4.10 na Katiba ya Kenya. Utekelezaji wa vipengele fulani vikuu vya Katiba utajenga mazingira inayohamasisha utekelezaji wa mwongozo wa OP 4.10 nchini Kenya. Utambuaji wa Wadau Wakuu 8 Wakati wa mikutano ya mashauriano na Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika, idadi fulani ya Mashirika Yasiyo ya Serikali (NGO) ilitambuliwa kuwa inafanya kazi na jamii za wenyeji. Pia ilibainika kwamba jamii nyingi hazikuwa zinafahamu wadau wote na majukumu ya asasi mbalimbali zinazofanya nao kazi. Miongoni mwa Washirazi/Wakifundi, Idara ya uvuzi, Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS), Reefolution, WCS, Serikali ya kaunti, Serikali ya taifa, Vitengo vya Kusimamia Fuo ndio wadau wenye shughuli nyingi. Katika eneo la Wasini, wadau waliotambuliwa na Wavumba Youth walijumuisha- wakfu wa elimu wa Wasini, Wasini youth tunaweza, waendeshaji wa boti Wasini, kundi la wanawake la Wasini, Wasini BMU, chama cha utalii wa kijamii Wasini na klabu ya soka ya Wasini. Miongoni mwa Waata katika eneo la Makinnon, serikali ya kaunti; KAPP; WWF; KWS; Wildlife works (inayoegemea utunzaji wa mazingira); Mashamba ya mifugo – Dokata ranch, Tara ranch, Mwabeji ranch, Kifungo ranch; KMC; KCDA; NDMA; Coast lobby; KALRO yalitambuliwa kuwa wadau wanaojulikana kwa baadhi ya wakazi. Katika Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika, kuna asasi za jadi kama vile wakuu wa vijiji na mabaraza ya wazee inayoitwa Dhuro, Abagaaza miongoni mwa Watta au mfumo wa gana miongoni mwa Wasaanye. Mifumo kama hiyo inapatikana miongoni mwa Makundi mengine Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika. Asasi hizi zina mamlaka ya kitamaduni ambayo inaheshimiwa sama katika jamii hizi ili kutoa fursa za kukabiliana na masuala ibuka miongoni mwa asasi mbalimbali katika Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yatakayotambuliwa kwenye mifumo ya usuluhishaji wa utata. Hali ya Kiuchumi na Kijamii 9 Kilimo na shughuli zinazohusiana na kilimo ndicho chanzo kikuu cha mapato kwa jamii nyingi za mashambani huku kikichangia asilimia 90 miongoni mwa jamii za pwani zilizohojiwa. Vyanzo vingine ni pamoja na shughuli zinazohusiana na utalii, asilimia tani, ajira asilimia mbili na kazi za kujiajiri mjini zikichangia asilimia mbili. Watu wanaoishi mashambani ni asilimia 72 (93,641) ya idadi ya watu wanaoishi katika kaunti. Sanasana, vijana hawana elimu ya kutosha, jambo linalosababisha ukosefu wa ajira kwa kutokuwa na ujuzi unaohitajika. Idadi kubwa ya nguvu kazi katika kaunti hizi haina ajira. Viwango vya ukosefu wa kazi ni vya juu sana katika kaunti huku takwimu za umaskini zikiwa zaidi ya asilimia 60. 10 Kuna mimea mingi inayokuzwa pwani ikiwemo mahindi, kunde, mihogo, mnazi, korosho, biksa, pamba, ufuta, machungwa, nyanya miongoni mwa mimea mingine inayokuzwa kwa kutegemea mvua. Mfumo huo umekuwa na athari kubwa kwa fursa za mapato, utoshelevu wa chakula na juhudi za kutokomeza umaskini katika kaunti ambapo mradi huu utafanywa. Idadi kubwa ya Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yaliyochaguliwa yapo katika hali ya mpito ya kujipatia riziki na kuishi, wengine wakiwa katika hali ya kitamaduni na wengine usasa kidogo. Hii ni kutokana na elimu duni na utangamano mdogo kutoka kwa jamii nyingine pamoja na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, kimazingira na kisiasa. Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yamebadilisha majukumu yao ya kijadi kutoka uwindaji na kukusanya maliasili na kuingilia kilimo cha kujikimu. Familia nyingi zinatumia visima, chemchemi au mabwawa kuwa vyanzo vikuu vya maji ya kunywa. Mahojiano ya Makundi Mahususi yaliyofanywa na Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yanaonyesha kwamba maji ndiyo changamoto kuu katika eneo ambako mradi utafanywa. Chanzo kuu cha chakula ni samaki, nyingine ni kilimo, ufugaji, biashara ndogondogo inayojumuisha uuzaji wa samaki na nazi. Samaki wengi huuzwa katika masoko ya karibu. Michakato inayozingatia utamaduni wakati wa kushauriana na Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika. Wakati wa kuandaa mradi 11 Ili kuboresha ujumuishaji na mashauriano bora na Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika, ni muhimu kwa mbinu zilizopo za mawasiliano zichukuliwe wakati mradi. Kufanya hivyo kutahakikisha kwamba makundi ya jamii ambayo kwa kawaida hukosa kuhudumiwa ipasavyo kama vile wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na makundi mengine yaliyo katika hatari ya kuathirika yanasikilizwa kikamilifu na maslahi na dhamira zao yanazingatiwa katika shughuli zote za mradi. Mikutano inafaa kuandaliwa kwa kushauriana na uongozi wa jamii kama vile machifu, manaibu wa chifu, wakuu wa vijiji na wazee wa jamii. Lengo na masuala makuu yatakayojadiliwa yanafaa kutajwa mapema kwa viongozi ili wafikishe kwa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika. Sehemu na muda mzuri kwa mkutano utakubaliwa kwa pamoja kwa mashauriano na viongozi. Tathmini ya kijamii ilibaini kwamba sauti ya wanawake ilikuwa haijitokezi wakati wa mikutano inayowajumuisha watu wote. Hii ina maana kwamba maoni yao huenda haitajumuishwa, isipokuwa mikutano maalum inayowalenga iandaliwe. Mikutano tofauti inayolenga wanawake iliandaliwa. Mikutano hii iliandaliwa chini ya makundi yaliyopo ya wanawake au mikutano inayowalenga wanawake katika makundi ya nyumba yaliyotambuliwa. 12 Idadi kubwa ya watu wa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika wakiwemo Waatha wa Kaunti za Tana River na Kilifi; Wakifundi/Wachwaka wa Kwale, Wasanye wa Lamu walipendelea mashauriano kupitia kwa wawakilishi na viongozi wa maeneo yao. Pia walipendelea watekelezaji wa mradi wa KEMFSED washauriane na Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika peke yao badala ya kujumuishwa pamoja na jamii zilizo na idadi kubwa ya watu ili sauti zao zisipotee. Wawakilishi wengi wa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika walitaja kwamba idadi kubwa ya watu wao walikuwa hawajui kusoma na kuandika. Kwa sababu hiyo, walipendekeza kuwe na mchakato mpana wa uhamishaji kabla ya mradi kutekelezwa. Idadi Jina la Kikundi cha Kata Kaunti Tarehe ya Wanaume Mazungumzo 1) Washiratzi VMG Vanga Kwale Tar. 12 Februari 2019 2) Wavumba VMG Wasini Kwale Tar. 14 Februari 2019 3) Tswaka /VMG Pongwe Kwale Tar. 14 Februari 2019 Kidimo/Shimoni 4) Watha VMG Mackinon Road Kwale Tar. 16 Februari 2019 5) Watha VMG Dabaso Kilifi Ter. 18 Februari 2019 6) Watha VMG Watamu Kilifi Tar. 18 Februari 2019 7) Watha Marereni Marereni Kilifi Tar. 20 Februari 2019 8) Saanye na Wanawake Kituo cha KEFRI, Lamu Tar. 22 Februari 2019 wa Aweer/VMG Mokoe 9) Saanye VMG Kipini Tana River Tar. 25 Februari 2019 Jina la Kikundi cha Kata Kaunti Tarehe ya Wanawake Mazungumzo 10) Kundi la Wanawake Wasini Kwale Tar. 14 Februari 2019 Wavumba/VMG 11) Kundi la Wanawake PongweKidimo/Shimoni Kwale Tar. 14 Februari 2019 Watswaka/VMG 12) Wanawake wa Watha Mackinon Road Kwale Tar. 16 Februari 2019 VMG 13) Wanawake wa Dabaso Kilifi Tar. 18 Februari 2019 Watha/VMG 14) Wanawake wa Watamu Kilifi Tar. 18 Februari 2019 Watha/VMG 15) Saanye na Wanawake Kituo cha KEFRI, Lamu Tar. 22 Februari 2019 wa Aweer/VMG Mokoe 16) Wanawake wa Kipini Tana River Tar. 25 Februari 2019 Saanye/VMG Tathmini inayotokana na mashauriano ya wazi, yaliyopangwa na kuridhiwa (FPIC) na wahusika wa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika. 13 Mashauriano ya wazi yaliyopangwa na kuridhiwa kwa ajili ya mradi huu yalichangia kupata uungaji mkono wa jamii, kwa makundi yaliyotengwa na yaliyo katika hatari ya kuathirika katika hatua yote ya upangaji na utekelezaji wa miradi ya KEFSED. Mpangilio huu unajumuishwa katika ngazi zote zinazohitaji kiasi kikubwa cha mashauriano na nyenzo za ushirikishaji katika hatua zote za kuandaa, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya mradi. Hatua 5 tofauti lakini zinazotegemeana na kiasi cha ushiriki zilitokea wakati wa mashauriano ya wazi, yaliyopangwa na kuridhiwa (FPIC) katika kaunti za pwani, nazo ni; uhamasishaji wa awali, kushiriki taarifa, mashauriano na kufanya uamuzi kwa pamoja. Vipengele hivi vyote wa ushiriki kamili na bora wa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika vilifanywa kwa namna inayoweza kueleweka kwa urahisi na jamii husika. Madhara na Manufaa yanayoweza kutokana na KEMFSED kwa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika 14 Matokeo makuu ya Tathmini ya Kijamii ilionyesha kwamba Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yanaunga mkono uimarishaji wa hali zao za kijamii na kiuchumi. Mradi huu uliungwa mkono sana wakati wa mashauriano. Shughuli za miradi zitatoa kipaumbele kwa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika katika maeneo yaliyobainishwa. Manufaa ya mradi pia yatajumuisha baadhi ya jamii ambazo hawapo katika Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika. Matokeo haya ya jumla yametajwa kimushtasari katika sehemu inayofuata. 15 Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yaliyohojiwa yanahisi kwamba kuboresha utawala na usimamizi wa uvuvi utasaidia katika kusuluhisha kutojumuishwa kwao ambako kumekuweko. Makundi mengi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yanahisi kwamba kwa sasa hakuna taarifa za kutosha kuhusu shughuli za sekta hiyo. Kuboresha usimamizi wa uvuvi wa baharini, ikiwa ni pamoja na uandaaji wa mfumo imara wa kufuatilia data ya uvuvi (FIMS) utasaidia katika upatikanaji wa taarifa kwa ajili ya usimamizi bora wa uvuvi. Mashauriano ya karibu na Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yataimarisha utambuaji na uwekaji wa vipaumbele katika utekelezaji unaohusu Mipango ya Kuboresha Uvuvi (FIPs). Kwa hakika, Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yanahisi kwamba hayana ujuzi na teknolojia inayofaa uvuvi wa maji makuu, na kwamba kipaumbele kinafaa kuelekezwa katika kusaidia wavuvi wadogo wadogo kutoka katika mradi wa FIP na kuingia katika miradi ya Kutathminiwa na Kupata Vyeti Kamili. Kadhalika kulikuwa na mtazamo wa kukubali mpango wa kuboresha usimamizi wa uvuvi wa karibu na ufuo. Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika pia yalikaribisha ushirikiano na mipango ya Kitaifa ya Usimamizi wa Uvuvi (FMP) na kwa ajili ya uvuvi na uundaji wa Maeneo ya Usimamizi wa Pamoja (JCMA) inayozijumuisha jamii za karibu. 16 Kwa upande mwingine, tathmini hii ya kijamii imeonyesha kwamba kwa kiwango kikubwa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yanategemea maliasili, hasa ya misitu na wanyamapori kujikimu. Wanategemea misitu kupata asali, matunda, dawa, kuni na makaa. Jamii hizi pia hutumia misitu kuabudu na kufanya matambiko. Kwa hivyo Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yanaweza kupata madhara yakikatazwa au kuzuiwa kufikia misitu kwa sababu rasilimali ya misitu inachangia sehemu kubwa ya maisha zao. Isitoshe, Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yalilalamika wakatia wa tathmini ya kijamii kwamba kwa sasa yanatengwa na mamlaka kama vile Shirika la Huduma kwa Wanyamapori, Mamlaka ya Usimamizi wa Misitu n.k katika usimamizi wa maliasili iliyo katika jamii zao. Wana wasiwasi hasa kwamba misitu itaisha pamoja na wanyama licha ya kwamba serikali imewaajiri maafisa zaidi wa misitu na wanyamapori. Kwa upande mwingine, mashirika ya kiserikali yanahitaji usaidizi wa ziada ili kuhakikisha utumiaji endelevu wa rasilimali, hasa mitindo inayohusisha jamii ili kupata usaidizi na kukabiliana na hisia ya kutengwa kwa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika. 17 Hatari kubwa ya kijamii ni kutojumuishwa kwa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika. Hatari za kijamii zinazoweza kutokea wakati wa utekelezaji wa mchakato huu unajumuisha: (i) uwezekano wa watu wa tabaka la juu katika jamii na kaunti kuingilia mradi na kuyaondoa makundi yaliyolengwa; (ii) kutojumuishwa kwa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika kwa sababu yanakosa uwakilisha katika ngazi mbalimbali za shughuli za jamii. Athari hizi zitakabiliwa kwa njia zifuatazo: uratibu wa mradi hivi kwamba katika mwaka wa kwanza uzingatie kujenga uwezo wa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika katika ngazi ya jamii, yawe na ujuzi wa kushawishi na kutetea ili kuelewa na kuchangia katika michakato ya utekelezaji wa miradi kwa lengo la kuhakikisha uwajibikaji wa kijamii. Masimulizi ya ufanisi kuhusu Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika 18 Katika maeneo yote ya Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yaliyotembelewa kuna shauku na matarajio makuu katika utekelezaji wa mradi. Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yanatazamia uungaji mkoni na kushiriki pakubwa katika utekelezaji wa miradi. Baadhi ya changamoto zilizotambuliwa kama vile migogoro ndani na kati ya jamii hazipo katika Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika eneo la pwani pekee. Mizozo kama inayohusu maliasili, yaani usimamizi (wengine walitaka kuanzishwa kwa kundi tofauti la usimamizi); mizozo ya mipaka, mizozo inayohusu kutotii sheria, na maofisa wanaofaa kusimamia utekelezaji wa sheria katika maeneo yenye maliasili kama vile KWS, KFS na KWS ni masuala ya kawaida katika maeneo mengine ya Kenya. Nia kuu ya Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika inahusu ushiriki wa moja kwa moja katika ngazi zote za utekelezaji ili wasiachwe nje, yaani katika ngazi ya jamii, kutumia mseto wa utawala wa jadi na wa viongozi wa kijiji kwa kiasi kikubwa inavyowezekana. 19 Utambuzi wa mbinu za kutumia kubashiri na kuepuka hatari na athari; katika matukio yasiyoepukika, punguza hatari na athari kuwa katika viwango vinavyokubalika; Baada ya kupunguza hatari na athari, idhibiti; pale athari kubwa inapobakia, fidia au lipia, pale ambapo inawezekana kiufundi na kifedha, hakikisha kwamba Jamii za Watu Asili inapokea manufaa yanayofaa Kijamii chini ya Mradi 20 Kupitia mashauriano kadhaa, Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yalipendekeza hatua kadhaa zinazofaa kuhakikisha kwamba yananufaika maendeleo yanayotokana na miradi. Watu wa Asili na Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yaliyohojiwa yamependekeza jinsi ya kuboreshewa uwezo ili kuwa na mchango wa maana na kunufaika na KEMFSED. Mikakati hiyo inajumuisha: • Kuongeza upatikanaji wa fursa za kujiajiri kupitia uwekezaji katika huduma za msingi, kujenga ujuzi wa ujasiriamali kwa watu wa Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika; • Uboreshaji wa ujuzi katika biashara na mafunzo kuhusu ustawi wa binafsi na wa kijamii; • Katika mashauriano yote na Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika, ilikuwa dhahiri kwamba wanapoteza utambulisho wao wa kijamii wanapojaribu kuingiliana na jamii zingine zilizo na wasemaji wengi na utamaduni kwa sababu ya mabadiliko ya kijamii. Utumiaji wa lugha za asili wakati wa kuwasiliana na Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika unaweza kusaidia kujenga ukuruba na wao. • Kadri wanavyojihusisha zaidi na zaidi na mradi unaopangwa, ufahamu wa haki zao na upekee wa utamaduni wao unafaa kukuzwa ili waweze kudumisha utambulisho na umoja wao. Hili linaweza kufikiwa kwa kuzingatia haki zao za kimaendeleo, uwakilishi, kusikilizwa katika ngazi mbalimbali za utawala, kulinda urithi wao wa kijamii ikiwemo lugha na kushiriki katika uongozi. Jinsi Makundi Yaliyotengwa na Yaliyo katika Hatari ya Kuathirika yatafaidika na vipengele vyote vya mradi: Kipengele cha 1 – Kuboresha Utawala na Usimamizi wa Uvuvi wa Baharini. 21 Hiki kitazingatia kuboresha usimamizi wa uvuvi wa baharini katika mipaka ya Kenya. a) Kipengele kidogo 1.1: Kuboreshwa kwa utawala wa uvuvi na uchumi wa baharini. Kipengele hiki kidogo kitazingatia kuboresha utawala na usimamizi wa uvuvi, kurekebisha sera na sheria za uvuvi na kuimarisha ufuatiliaji na upelelezi. Kipengele hiki kidogo pia kitazingatia kuboresha usimamizi wa uvuvi wa baharini, ikiwa ni pamoja na uandaaji wa mfumo imara wa kufuatilia data ya uvuvi (FIMS) utakaosaidia katika upatikanaji wa taarifa kwa ajili ya usimamizi bora wa uvuvi. Itakapobainishwa, maeneo ya uvuvi yatakayopewa kipaumbele yatazingatiwa kupokea misaada inayoingiliana na Mipango ya Kuboresha Maeneo ya Uvuvi (FIP), lengo likiwa kuboresha maeneo hayo yawe na usimamizi utakaohakikisha manufaa endelevu kwa jamii husika. Mradi pia utaunga mkono uandaaji wa Mipango ya Utekelezaji wa Kitaifa kwa ajili ya papa, ndege na uvuvi Haramu, Usioripotiwa wala Kudhibitiwa (IUU). b) Kipengele kidogo 1.2: Kuboresha usimamizi wa uvuvi wa karibu na fuo. Kipengele hiki kidogo kitaimarisha usimamizi wa maeneo ya uvuvi yaliyo karibu na fuo na kutekeleza Mipango ya Usimamizi wa Uvuvi (FMP). Kwa kushirikiana na Mipango ya kitaifa ya Usimamizi wa Uvuvi, Maeneo mapya ya Usimamizi wa Pamoja (JCMA) yataandaliwa huku usimamizi wa maeneo yaliyopo ukiimarishwa. Mradi pia utaunga mkono utekelezaji wa Maeneo ya Usimamizi wa Kushirikiana (CMA) ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mikakati ya Ufuatiliaji, Udhibiti na Upelelezi (MCS) na utoaji wa zana na ufundi unaohitajika kwa ajili ya Ufuatiliaji, Udhibiti na Upelelezi. c) Kipengele kidogo 1.3: Ustawi wa miundomsingi kwa ajili ya usimamizi wa maeneo ya uvuvi. Kipengele hiki kidogo kinajumuisha ustawi wa miundomsingi inayonuiwa kusaidia katika usimamizi wa maeneo ya uvuzi katika ngazi ya kitaifa na kaunti. Kimahususi, kinajumuisha ujenzi wa ofisi za Idara ya Huduma za Uvuvi nchini (KeFS) jijini Nairobi na Kituo cha Kitaifa cha Mafunzo ya Uvuvi wa Baharini katika Kaunti ya Kwale. Mifano ya miundomsingi ya uvuvi inayoweza kuboreshwa ni pamoja na ofizi za kaunti za uvuvi na upanuzi wa Chuo cha Mafunzo ya Baharini cha Bandari jijini Mombasa. Kipengele cha 2 – Kuwezesha Uwekezaji Endelevu katika Uvuvi wa Baharini na Kilimo cha majini. 22 Hiki kitaanzisha Huduma ya Ustawi wa Biashara Ndogondogo na za Kati (SME-DS) utakaotoa ujuzi unaopatikana kwa urahisi kwa wajasiriamali, Biashara ndogo na za kati na mamlaka katika kaunti za pwani, vilevile itaongeza thamani inayopatikana kutokana na uvuvi na maliasili za baharini kwa kuwekeza katika miundomsingi ya umma, kama vile barabara, umeme, usambazaji wa maji, yote haya yakiunganishwa na mfumo wa thamani na uwekezaji wa binafsi. a) Kipengele kidogo 2.1: Huduma ya Ustawi wa Biashara Ndogondogo na za Kati (SME- DS) kwa Jamii za Pwani. Zabuni itatolewa kwa shirika la Huduma ya Ustawi wa Biashara Ndogondogo na za Kati (SME-DS), shirika hilo litakuwa na wataalamu wa masuala ya ustawi wa biashara ndogondogo na itahudumia jamii zilizo katika pwani ya Kenya. Wajuzi hawa watapeleka huduma zao katika Vitengo vya Usimamizi wa Fuo (BMU) na kwa wakazi wa pwani wanaotaka kukuza au kupanua biashara zao zinazohusiana na uvuvi, watatoa usaidizi wa kiufundi unaohitajika, huduma za uchanganuzi, uhamasishaji na huduma za kusambaza ufahamu. Huduma ya Ustawi wa Biashara Ndogondogo na za Kati (SME-DS) pia itatambua hatari za kimfumo au masuala yanayozuia miradi tarajiwa kuwa tayari kwa uwekezaji na itapendekeza hatua za ukombozi zinazohitajika ili kuondoa au kudhibiti hatari kama hizo. Mafundisho na maelekezo kuhusu kupata vyanzo vilivyopo na vinavyoibuka vya ufadhili pia yatajumuishwa. Kipengele hiki kidogo pia kutasaidia biashara ndogondogo na za kati ambazo zinataka kubuni huduma za kuongeza thamani na kuwa na mfumo wazi zaidi wa biashara ya vyakula vinavyotoka baharini. Isitoshe, mradi pia utatoa usaidizi wa kiufundi kuongoza uanzishaji na utekelezaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Biashara ya Samaki nchini Kenya. b) Kipengele kidogo 2.2: Kuboresha Miundomsingi ya Uvuvi na Maliasili ya Baharini kwa lengo la kustawisha mfumo wa Thamani. Kipengele hiki kidogo kitazingatia mianya iliyotambuliwa na kaunti katika miundomsingi ya umma (maji, umeme, uchukuzi) inayokwaza fursa za uwekezaji katika uvuvi uchumaji wa maliasili ya baharini. Ili kuhakikisha kwamba uwekezaji wote unaweza kutetewa, kusaidia uwekezaji saidizi wa binafsi na kupunguza uwezekano wa uvuvi kupita kiasi, miradi yote ya umma inayohusiana na mfumo wa thamani unaopendekezwa na kaunti utatokana na ramani na mipango ya kaunti ya uvuvi na utumiaji wa maliasili ya baharini. Hatari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi yatazingatiwa katika uwekezaji wote wa miundomsingi. Kipengele cha 3 – Uwezeshaji na Uimarishaji wa Upatikanaji wa Riziki wa Jamii za Pwani. 23 Kipengele hiki kitazingatia kuboresha upataji riziki kwa familia masikini miongoni mwa jamii za pwani, hilo likiwa lengo kivyake, na pia ili kuwasaidia wavuvi kutii mipangilio ya usimamizi wa uvuvi. Utaratibu jumuishi unaolenga ustawi wa mbinu mbadala wa uchumaji riziki utaandaliwa, kufuatiliwa, kwa kiasi fulani kwa kushirikiana na washirika wapya au waliopo wanaohusika katika biashara ya kilimo au kilimo cha baharini, mipango ya kilimo cha ukodishaji inayofaidisha miradi midogo midogo. Kwa ujumla, miradi midogo ya uchumaji wa mapato, inayotekelezwa na watu binafsi (midogo) au makundi ya biashara ndogo, itasaidiwa kupitia utoaji wa ruzuku, usaidizi wa kiufundi na mafunzo ya ujuzi na ujasiriamali. a) Kipengele kidogo 3.1: Kuboresha Upataji Riziki kwa Jamii za Pwani. Kipengele hiki kidogo kinajumuisha hazina itakayofadhili miradi inayostahili kupitia njia tatu tofauti: i) Ufadhili wa miradi midogo ya riziki kwa mashirika madogo yanayohudumu katika eneo la pwani; ii) Ufadhili kwa miradi ya kijamii na kimazingira (mtaji asili ); na iii) Ufadhili wa mtaji kwa vikundi vya akiba na mikopo vijijini. b) Kipengele kidogo 3.2: Huduma za Usaidizi kwa Uboreshaji wa Upataji wa Riziki na Uimarishaji wa Uwezo. Kipengele hiki kidogo kitatekelezwa na kila kaunti na kitatoa huduma za usaidizi na uimarishaji wa uwezo ili kunufaisha makundi yanayotaka kutoa na kusaidia shughuli zilizo katika kipengele kidogo cha 3.1 ikiwemo: i) utoaji wa Usaidizi wa Huduma na Ufundi ili kutambua wapokeaji wa ufadhili na kusaidia katika kuandaa, kusimamia na kufuatilia miradi midogo; ii)Kutoa mafunzo ya kiufundi na ujasiriamali kwa wanaopokea ruzuku na wafanyabiashara wadogo wadogo; iii) Miradi ya vikundi vya akiba na mikopo vijijini; na iv) Ufadhili wa elimu kwa mafunzo rasmi, mafunzo ya kiufundi na elimu ya darasani. Kipengele cha 4 – Usimamizi wa Mradi. 24 Kipengele hiki cha 4 kitafadhili usaidizi wa ziada wa usimamizi wa miradi katika ngazi ya kitaifa na kaunti ili kuhakikisha uratibu na utekelezaji wa shughuli za mradi kwa wakati. Kwa umahususi, kitasaidia katika ufuatiliaji na ushirikishaji wa mradi ikiwa ni pamoja na kuratibu shughuli za Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mradi (NPSC) na Kamati ya Ushauri wa Kiufundi (PTAC); kuanzishwa na utekelezaji wa Kitengo cha Uratibu wa Mradi (PCU) katika ngazi ya kitaifa na Vitengo vya Utekelezaji wa Mradi katika ngazi ya kaunti, pamoja na utoaji wa zana, usimamizi wa amana, ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa mahesabu na uhasibu wa ndani na nje, udhibiti wa ubora na mifumo ya uhakikishaji; usimamizi wa mifumo ya kimazingira na kijamii pamoja na ukaguzi wa kiufundi inavyohitajika. Kipengele hiki pia kitafadhili uandalizi na utekelezaji wa mkakati wa mawasiliano na utekelezaji wa Ufuatiliaji na Tathmini. Mifumo ya Ufuatiliaji na Tathmini itafaa kutekelezwa ili kupata data kuhusu hatua za nyanjani na za kifedha, utendakazi wa shirika linalotekeleza na asasi/watoa huduma wengine pamoja na matokeo na ufanisi kwa mujibu wa yanayowekezwa na matokeo. Isitoshe, itasaidia kuanzisha Mfumo wa Kusuluhisha Malalamiko na kuhakikisha ushirikishaji wa wananchi.